Wanafunzi wa kike wa Hawzah ya Hazrat Zainab (sa) Kigamboni, Dar es Salaam, wameendelea kuhuisha kisomo cha Dua ya Kumail bin Ziyad, wakijengwa katika malezi ya kiroho, unyenyekevu mbele ya Mwenyezi Mungu na umuhimu wa dua katika maisha ya kila siku.

17 Julai 2026 - 14:04

Kwa Mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) –ABNA– Wanafunzi wa kike wa Hawzah ya Hazrat Zainab (sa) iliyopo Kigamboni, Dar es Salaam, wameendelea kuhuisha kisomo cha Dua ya Kumail bin Ziyad, moja ya dua mashuhuri zilizopokewa kutoka kwa Amirul Muuminin, Imam Ali bin Abi Talib (as).
 
Kisomo hicho ni sehemu ya programu za malezi ya kiroho zinazolenga kuwajenga wanafunzi katika kumtegemea Mwenyezi Mungu, kujitathmini, kutubu kwa dhati, kuimarisha uhusiano wao na Mola Mtukufu na kuifanya dua kuwa sehemu ya maisha yao ya kila siku.
 
Dua ya Kumail ni miongoni mwa hazina kubwa za maarifa ya Kiislamu. Inamfundisha Mwislamu namna ya kuzungumza kwa unyenyekevu na Mola wake, kuomba msamaha, rehema, uongofu na nguvu ya kutekeleza amri za Mwenyezi Mungu. Vilevile humkumbusha mwanadamu udogo wake mbele ya Muumba na ukubwa wa rehema za Allah (swt).
 
Malezi ya Hawzah ya Hazrat Zainab (sa) yanatoa nafasi maalumu kwa ibada, dua, Qur'ani Tukufu na maadili ya Kiislamu, yakilenga kuwaandaa wanafunzi kuwa wanawake wenye elimu, uchamungu na uwezo wa kuitumikia jamii kwa hekima na uadilifu.
 
Katika mafundisho ya Ahlul-Bayt (as), Dua ya Kumail imepewa nafasi ya pekee. Imepokewa kutoka kwa Kumail bin Ziyad kwamba Imam Ali (as) alimfundisha dua hii na akamwambia:


 
يَا كُمَيْلُ، إِذَا حَفِظْتَ هَذَا الدُّعَاءَ فَادْعُ بِهِ كُلَّ لَيْلَةِ جُمُعَةٍ، أَوْ فِي الشَّهْرِ مَرَّةً، أَوْ فِي السَّنَةِ مَرَّةً، أَوْ فِي عُمْرِكَ مَرَّةً، تُكْفَ وَتُنْصَرْ وَتُرْزَقْ، وَلَنْ تُعْدَمَ الْمَغْفِرَةَ.


 "Ewe Kumail! Ukiihifadhi dua hii, isome kila usiku wa Ijumaa; au angalau mara moja kwa mwezi, au mara moja kwa mwaka, au hata mara moja katika maisha yako. Ukifanya hivyo utalindwa, utasaidiwa, utaruzukiwa, na hutanyimwa msamaha wa Mwenyezi Mungu."
 
Riwaya hii inaonesha nafasi adhimu ya Dua ya Kumail katika kujenga maisha ya kiroho ya Muislamu. Kwa kuendelea kuisoma kwa ikhlasi na kutafakari maana zake, waumini huimarisha Tawakkul yao kwa Mwenyezi Mungu,  huongeza unyenyekevu, na hupata nguvu ya kukabiliana na changamoto za maisha kwa matumaini, subira na imani thabiti.

Maoni yako

You are replying to: .
captcha